Thursday, September 8, 2011

Mfumo mpya wa usambazaji wa dawa MSD bado si wa uhakika!

Taarifa kwa Umma


TATIZO la upatikanaji au uhaba wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya huduma ya Afya vya Umma huchangia kwa kiasi kikubwa vifo kwa wagonjwa nchini Tanzania hasa wale wanaoishi vijijini.Sababu kubwa inayochangia uhaba wa madawa na vifaa tiba ni mfumo mbovu wa usambazaji.
Katika mfumo wa zamani wa usambazaji, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilikuwa ikitoa vifaa na dawa kwa ngazi ya wilaya na kisha ngazi ya wilaya kusambaza katika vituo vya afya kwa kuzingatia mahitaji yao waliyoainisha. Mfumo huu ulikuwa na mapungufu ya ucheleweshaji wa kupokea vifaa tiba na dawa, kupotea au kupokelewa vikiwa vimebakiza muda mfupi wa matumizi au muda wake wa matumizi kuisha kabisa. Mfumo huo pia ulilalamikiwa na wadau mbalimbali wakiwemo watoa huduma za afya na wabunge kutokana na kusababisha upotevu mkubwa wa rasilimali na kwa kuwa umekuwa ukipuuzia malalamiko ya wananchi.
Katika mwaka wa fedha 2010/2011 MSD ilianzisha mfumo mpya wa kusambaza madawa na vifaa tiba mojakwamoja kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi katika vituo vya huduma za afya vya serikalini. Katika majaribio ya mfumo mpya wa usambazaji yaliyofanyika katika mkoa wa Tanga kuanzia mwezi wa pili 2010, mfumo huu mpya ulionekana kuleta ufanisi katika usambazaji. Pia iligundulika kuwa baadhi ya vituo vya afya ambavyo vilikuwa havijaanza kutoa huduma vilikuwa vinapata dawa na vifaa tiba kutoka MSD kwa kupitia waganga wakuu wilayani.
Sikika ilifurahishwa na maboresho yaliyotokana na mfumo huu mpya. Hata hivyo baada ya utekelezaji wa mfumo huu mpya wa usambazaji, bado changamoto zilezile zimejitokeza. Mfano katika wilaya ya Kilombero kulikuwa na malalamiko kwamba vituo vingi vya huduma vimechelewa kupokea dawa na vifaa tiba vilivyoagiza, pia pesa wanazotoa haziendani na idadi ya dawa na vifaa tiba vinavyopolekwa kwenye vituo. Zaidi ya hapo, hakuna mfumo wa mawasiliano rasmi kutoka MSD kwenda kwenye vituo husika pale inapokuwa kwamba vituo vimetumiwa madawa au vifaa pungufu kulingana na kiasi cha fedha waliyotengewa.
Sikika inaamini kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati katika vituo vya huduma ya Afya vya Umma unaweza kuokoa maisha ya wananchi wengi nchini na hivyo, hilo inabidi liwe ndiyo lengo kuu la uwepo wa MSD.
Sikika inaisisitiza MSD kuboresha mfumo wake mpya ili kuepuka changamoto zilezile za mfumo wa zamani. Mfumo mpya lazima uwe na ubora na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa katika vituo vya afya.
Sikika pia inatoa wito kwa MSD kuboresha mfumo wa mtiririko wa mawasiliano kwenda na kutoka katika bohari ndogo za kanda na katika vituo vya afya ili kuimarisha mfumo mpya. Hii itawezekana tu kama kila muhusika katika kufunga na kusambaza dawa na vifaa atatimiza wajibu wake ipasavyo. Karatasi za kuagizia dawa na vifaa zinapaswa kuonesha kinachotoka na kinachopokelewa na ninani muhusika wa kuwasiliana naye kama kuna malalamiko katika vituo vya huduma.
Sikika inatoa wito pia kwa Bohari Kuu ya Dawa nchini katika kutekeleza azma ya kuondokana na mfumo mbovu wa usambazaji dawa unaosababisha usheleweshaji wa kupokea na upotevu wa vifaa tiba ili kunusuru maisha ya wananchi. Wizara ya Afya pia ni lazima ihakikishe kuwa MSD inaanzisha kitengo cha kushughulikia malalamiko toka kwa wateja wake ili iweze kuyafanyia kazi malalamiko yote yanayohusiana na usambazaji wa dawa na vifaa katika vituo vya afya.



Mr. Irenei Kiria
Mkurugenzi wa Sikika, P.O.Box 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz, Tuvoti: www.sikika.or.tz

No comments:

Post a Comment